
Akitoa taarifa ya matokeo ya mtihani huu, tarehe 23 Januari, 2025, Jijini Dodoma, Msajili wa Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania Bi. Agnes Mtawa, amebainisha kuwa, jumla ya watahiniwa 5125 walifanya mtihani huu, ambapo watahiniwa 3281 (64%) wamefaulu mtihani na watahiniwa 1844 (36%) hawakuweza kufikia kiwango cha ufaulu kinachokubalika.
Aidha, Matokeo hayo yanapatikana kwenye akaunti ya kila mtahiniwa iliyopo kwenye mfumo wa kumbukumbu wa Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania (TNMCIS), Hivyo, kila mtahiniwa anatakiwa kuingia katika mfumo wa Baraza https://tnmcis.tnmc.go.tz. na kuweza kuona matokeo yake.
Mtihani wa usajili na leseni ni kwa mujibu wa Sheria ya Bunge ya Uuguzi na Ukunga “The Nursing and Midwifery Act, 2010” Kifungu cha (6) (a) na (o) iliyounda Baraza la Uuguzi na ukunga nchini
Baraza linawapongeza wale wote waliofaulu na kupata sifa za usajili na leseni na kwa wale walioshindwa kufikia viwango vya ufaulu vinavyokubalika, watajulishwa muda wa kurudia mtihani huu.
Ikumbukwe kuwa, Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania TMNC ni mamlaka ya kisheria inayosimamia wanataaluma na taaluma za Uuguzi na Ukunga Tanzania, chini ya Sheria ya Uuguzi na Ukunga ya mwaka 2010 na kanuni zake ili kuhakikisha kuwa huduma zinazotolewa na wauguzi na wakunga nchini zina kiwango kinachokubalika na salama kwa jamii.