Waziri wa Afya Ummy Mwalimu ametaka Mabaraza ya Madaktari na Wauguzi kuwachukulia hatua Mganga na Muuguzi waliosababisha kifo cha mjamzito Mariam Zahoro kilichotokea Kituo cha Afya Kabuku, Wilaya ya Handeni mkoani Tanga.
Mwalimu amesema Mariam hakufariki kwa ajili ya kukosa kiasi cha shilingi 150,000, bali ni kwa ajili ya uzembe wa baadhi ya wahudumu wa Afya kwa kushindwa kuwajibika kutokana na hali aliyokuwa nayo mgonjwa.
Ameyasema hayo Novemba 27, 2023 baada ya kupokea taarifa ya Tume iliyoundwa kuchunguza jambo hilo lililotokea Novemba 11, mwaka huu, kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Kituo cha Afya Kabuku, ambapo Tume imebaini wahudumu wawili ndiyo wenye makosa.
“Tunataka Mabaraza ya Madaktari na Wauguzi wachukue hatua kwa Daktari na Muuguzi walioshindwa kuwajibika,kosa la daktari ni kushindwa kufika kwa wakati tayari ameelezwa hali ya mjamzito ni mbaya,hata alipofika, alishindwa kuchukua hatua ya kumpeleka Hospitali ya Wilaya ya Handeni, Mkata baada ya kumkosa Muuguzi wa dawa za usingizi ili mgonjwa afanyiwe upasuaji lazima apewe dawa za usingizi,”ameeleza Mwalimu na kuongeza kuwa
“Kosa la Muuguzi ni kumueleza mgonjwa anatakiwa alipe 150,000 wakati huo sio utaratibu, kwani alitakiwa atoe huduma bila kudai fedha hizo hivyo nitangaze mjamzito hakupoteza maisha kwa ajili ya kukosa sh.150,000, bali ni kwa ajili ya uzembe wa baadhi ya wahudumu wa Afya,”.
Mwalimu amesema Sera ya Afya ya mwaka 2007 inamtaka mjamzito kupata huduma bila malipo, hivyo amepinga makubaliano yaliyofikiwa kwenye kata kati ya wahudumu wa Afya na watendaji akiwemo Diwani wa eneo hilo kupitisha kuwa mjamzito atatoa sh. 150,000 kwa ajili ya upasuaji.
Amesema anataka Mabaraza hayo yatoe maamuzi ndani ya wiki mbili, huku akiwaahidi wananchi hao kuwa wahudumu hao wawili hawatarudi Kabuku na kutaka hatua kali zichukuliwe dhidi yao iwe onyo kwa wengine.
Hata hivyo Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amekiri baadhi ya majengo kwenye kituo hicho yamechoka, na atatafuta fedha kujenga mengine.
Credit:Gazeti la Majira