THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA

TANZANIA NURSING AND MIDWIFERY COUNCIL

Wataalamu wa Afya wametakiwa kutumia taaluma na ueledi walionao kwa kuzingatia mafunzo ya chati uchungu ili kupunguza idadi ya vifo vya Mama na Mtoto ambavyo vimekuwa vikijitokeza.

Hayo yamesema na Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Daniel Mzee, wakati akizungumza na Madaktari pamoja na Wauguzi Wakunga katika mafunzo ya Chati Uchungu yanayofadhiliwa na USAID kupitia mradi wa Afya Yangu yanayoendelea Mkoani Shinyanga.

Dkt. Mzee amewaeleza wataalamu hao kuwa mafunzo hayo yana umuhimu mkubwa katika kuboresha Afya ya Mama na Mtoto, hivyo na ili kufanyika vizuri hawana budi kuyazingatia kwa kuyafanyia kazi kwa makini.

“Tusikilize vizuri mafunzo na tuzingatie miongozo kwa lengo la kupunguza vifo vya mama na mtoto. Bado kasi haijawa ya kuridhisha, lakini hapa tulipofikia ni pazuri hivyo tuendelee kupambana, Nina uhakika mtakapoenda kwenye maeneo yenu ya kazi mtatumia mafunzo haya kuwafundisha na wenzenu ili mboreshe huduma nzuri hususani katika kuokoa maisha ya mama na mtoto”, amesema Dkt. Mzee.

Kwa upande wake Mkunga Mbobezi kutoka Idara ya Huduma za Uuguzi na Ukunga Wizara ya Afya, Aziza Machanje, amesema Serikali imeelekeza kutolewa kwa mafunzo ya Chati Uchungu ambayo imeboreshwa zaidi kuzidi kukabiliana na changamoto zitokanazo na uzazi hasa kwa mama na mtoto.

“Chati Uchungu ni chati inayotumia kuangalia maendeleo ya mama mjamzito wakati wa kujifungua ili kujua maendeleo ya mama na mtoto tumboni, Tumeona umuhimu mkubwa wa kuwa nayo moja ili itumike nchini kote, na ndiyo maana Wizara imeamua kuandaa haya mafunzo kwa wataalamu wetu wa Afya”, amesema Machanje.

Credit: WAF

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *