THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA

TANZANIA NURSING AND MIDWIFERY COUNCIL

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. Jonh Jingu, amewaagiza Wasajili wa Mabaraza na Bodi za kitaaluma zilizochini ya Wizara ya Afya, kuimarisha na kusimamia mifumo ya Maadili ya kitaaluma na ya kazi kwa watumishi wa kada ya Afya, kwa kufika katika maeneo yao ya kazi badala ya kusubiri waletewe kesi mezani.

Katibu Mkuu, ametoa rai hiyo Februari 02.2024 alipofanya kikao kazi na Wasajili wa Mabaraza 12 na Bodi mbili zinazosimamia Taaluma na wanataaluma wa kada mbalimbali za Afya ikiwa ni pamoja na Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania(TNMC).

“Nendeni field, tuwe na mikakati ya kuwafikia watu wetu, fuatilieni namna ambavyo wanafanya kazi, kunabaadhi ya wataalamu wetu ni watukutu, hawazingatii Maadili kama vile kutibu kinyume na tiba inayotakiwa, kutoa siri za wagonjwa, lakini pia tuimarishe mafunzo ya kujiendeleza kitaaluma kwa wataalamu wetu wakiwa kazini (CPD), tusisubiri matatizo yatokee, tuwe (proactive)” alisistiza Katibu Mkuu.

Akizungumzia suala la ugatuaji wa madaraka, Katibu Mkuu Dkt. Jingu, amewataka Wasajili hao kugatua Madaraka kwa wasimamizi wa ngazi za mikoa RNO na RMO ili kupata usimamizi wa karibu katika kusimamia Taaluma na wanataaluma, lakini pia kuwajengea uwezo ili wawe na weledi na maarifa sahihi ya kutekeleza majukumu waliyokasimiwa kwa ufasaha.

“Lakini pia, tujitangaze ili tufahamike, tuhakikishe kuwa mabaraza yetu yanajulikana kwa umma, tujitangaze kwa kufafanua majukumu yetu ili wananchi watufahamu na wanapokuwa na jambo wajue wapi pakwenda” alitanabaisha.

Akihitimisha hotuba yake, amesema, pamoja na kwamba Mabaraza haya ni Mamlaka za kisheria, hazitakiwi kuwa kero kwa wawekezaji waliowekeza au wanaotaka kuwekeza katika Sekta ya Afya kwani Serikali imekuwa ikihamasisha uwekezaji katika Sekta hiyo, hivyo utekelezaji wa majukumu yao usiwe kero ya kuwakatisha tamaa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *