Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania linaendesha Kikao cha kawaida cha Baraza la Uuguzi na Ukunga cha robo ya tatu, kinatarajiwa kufanyika kwa siku mbili mfululizo tarehe 23 na 24/05/2024 kuanzia saa 03:00 asubuhi, katika ukumbi mdogo wa mikutano wa Jakaya Kikwete Jijini Dodoma
Kikao kinaendeshwa na Mwenyekiti wa Baraza Prof. Lilian Mselle, na wajumbe wengine 12 walioteuliwa na waziri wa Afya huku Msajili wa Baraza Bi. Agnes Mtawa akiwa ni katibu wa kikao hicho.
Kikao kinatarajia kuangazia Agenda kuu mbili, ambazo ni uendeshaji wa mashauri na kufanya maamuzi dhidi ya tuhuma 06 za uvunjifu wa maadili ya kitaaluma zinazowakabili wauguzi na wakunga kutoka mikoa ya Tanga, Morogoro, Geita, Pwani, Mara na Shinyanga.
Aidha, Agenda nyingine ni kupokea na kujadili utekelezaji wa majukumu ya kurugenzi na vitengo vya Baraza kwa kipindi cha robo ya tatu ya mwaka wa Fedha 2023/2024.
Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania ni Mamlaka ya kisheria inayosimamia wanataaluma na taaluma ya Uuguzi na Ukunga ili kuhakikisha huduma zinazotolewa na wauguzi na wakunga hapa nchini ni salama kwa jamii.