Serikali kupitia Wizara ya Afya imetenga fedha katika Bajeti ya Mwaka 2024/25 kwa ajili ya kujenga chuo kikubwa na cha kisasa cha Afya – Mirembe cha uuguzi na ukunga kitakachokua na vifaa vya kisasa ambacho kitatoa wataala wa kutosha katika Sekta ya Afya.
Waziri Ummy amesema hayo leo Juni 12, 2024 alipofanya ziara katika chuo cha Afya – Mirembe kwa kujionea hali ya chuo hicho pamoja na kuzungumza na wanafunzi wa chuoni hapo.
“Serikali imeona ipo haja ya kuongeza idadi ya wataalam wa Afya ya akili nchini Tanzania kwa kujenga Hospitali kubwa pamoja na kuanzisha kozi ya mafunzo ya diploma ya juu ya uuguzi katika afya ya akili ili kuboresha upatikanaji wa wataalam wa afya nchini ambapo wanafunzi watakao soma kozi hiyo kunufaika na mikopo kutoka Bodi ya Mikopo Tanzania.” Amesema Waziri Ummy
“Lengo letu ni kuhakikisha tunazalisha wataalam wa Afya ikiwemo wauguzi na wakunga wenye sifa pamoja na ujuzi walio pikwa wakapikika na wanaozingatia maadili ya kazi.” Amesisitiza Waziri Ummy
Amesema, lengo la Serikali kupitia Wizara ya Afya ni kuanzisha Diploma ya juu kwenye masuala ya saikolojia tiba ili kusaidia watu wenye changamoto za afya ya akili kutokana na ongezeko la idadi ya watu wenye changamoto hizo.
“Tunaona ongezeko la idadi ya watu wenye changamoto za afya ya akili ambapo takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonesha kuwa katika kila watu Nane mtu Mmoja ana changamoto za afya ya akili.” Amesema Waziri Ummy
Waziri Ummy amesema Mwaka 2023 Wizara ya Afya ilifanikiwa kuanzisha shahada ya kwanza ya sayansi ya saikolojia tiba ‘Clinical Psychology’ katika chuo kikuu cha Afya na Sayansi shirikiahi Muhimbili (MUHAS).
Naye mkurugenzi wa Huduma za Uuguzi na Ukunga nchini Bi. Ziada sellah amewataka wanafunzi wa kada ya Uuguzi na Ukunga kizingatia maadili ya taaluma ili waje kuwa watoa huduma bora
Aidha, Msajili wa Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania Bi. Agnes Mtawa amebainisha kuwa ni mwiko kwa mtoa huduma za Uuguzi na Ukunga kutoa huduma pasipo kusajiliwa na Baraza hivyo ni vyema kuzingatia usajili kwa kila hatua katika kada hiyo.