Msajili wa Baraza la Uuguzi na Ukunga nchi Tanzania Bi. Agnes Mtawa akiwa na menejimenti yake, tarehe 06 Agosti 2024 aliwasilisha taarifa ya utendaji kazi wa Baraza mbele ya kamati ya Bunge inayosimamia sekta ya Afya na UKIMWI kupitia kikao kilichofanyika katika ukumbi mdogo wa Bunge Bungeni Jijini Dodoma.
Kamati hiyo ambayo iliongozwa na Mwenyekiti wake Mhe. Elibariki Kingu (MB) kwa ujumla wamefurahishwa na wasilisho la Msajili na kubainisha kuwa wasilisho hilo limesababisha wabunge wa kamati hiyo kulifahamu vema Baraza pamoja na mipango yake.
“Kwa kweli tuwapongeze sana Baraza kwa utendaji mzuri wa kazi na pia nikupongeze sana Dada Agnes, kwa kweli unaonesha jinsi gani unaijua taasisi unayoiongoza, CMO huyu ni hazina ya Wizara ya Afya endeleeni kumtumia kwa mambo mengi” Alisema Mwenyekiti wa kamati hiyo Mhe. Elibariki Kingu.
Aidha, baada ya wasilisho hilo wabunge ambao ni wajumbe wa kamati hiyo, waliuliza maswali mbalimbali yenye nia ya kulielewa Baraza na majukumu yake, mipango yake na maendeleo yaliyofikiwa tangu kuanzishwa kwake mwaka 1953, maswali yote yalijibiwa vema na Msajili na hata Mwenyekiti wa kamati kumpongeza kwa umahiri wa kufafanua.