TNMC ikiwakilishwa na Msajili Bi. Agnes Mtawa, pamoja na maafisa waandamizi ambao ni Salome Kassanga na Irene Chilewa, imeshiriki Mkutano wa kimataifa wa kisayansi unaoratibiwa na jumuiya ya ECSACON nchini Lesotho kuanzia tarehe 11 hadi 13 Septemba 2024 kwa lengo la kubadilishana elimu, uzoefu na kuboresha utoaji huduma katika sekta ya Afya kwa nchi wanachama.
Mkutano huo unaotoa fursa kwa washiriki kujifunza, kufahamiana na kubadilishana uzoefu katika utoaji wa huduma za Afya, uelimishaji wa Uuguzi, Wadhibiti, Serikali na vyama vya kitaaluma , huandaliwa kila baada ya miaka miwili katika nchi mabalimbali wanachama ambapo Tanzania ni miongoni mwa nchi hizo.
Jumla ya nchi 16 wanachama zinazounda jumuia ya ECSACON ni pamoja na Tanzania, Botswana, Kenya, Lesotho, Malawi, Mauritius, Msumbiji, Namibia, Rwanda, Seychelles, Afrika Kusini, Sudan Kusini, Swaziland, Uganda, Zambia na Zimbabwe.
ECSACON ilianzishwa mwaka wa 1990 kama chombo cha utekelezaji cha iliyokuwa Sekretarieti ya Jumuiya ya Madola ya Afrika Mashariki, Kati na Kusini (CRHCS-ECSA) katika eneo la Uuguzi na Ukunga chenye makao yake makuu Jijini Arusha nchini Tanzania, ambayo sasa inajulikana kama Jumuiya ya Afya ya ECSA (ECSA HC) ikiwa na majimbo 14 ya kikanda. Pia, ni mojawapo kati ya vyuo vitano vya ECSA-HC ambavyo ni COSECSA ,CANECSA, COPECSA na ECSACOG.