Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania (TNMC) leo 11.10.2024 limezindua mfumo wa mawasiliano ya huduma kwa wateja utakao tumika kuwasiliana na umma hususani wadau wake wakuu ambao ni wauguzi na wakunga ndani na nje ya nchi ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha kilele cha wiki ya huduma kwa wateja.
Wiki ya huduma kwa wateja ilianza tarehe 07 Oktoba 2024 na kumalizika leo Oktoba 11, 2024 ikiwa imebeba kauli mbiu inayosema “Huduma zenye ubora na za kiwango cha juu zaidi”.
Akizindua mfumo huo wa mawasiliano katika ofisi za Baraza Jijini Dodoma kaimu Msajili Bi. Jane Mazigo, amesema kwa sasa Baraza litakuwa linatumia namba moja tu ya mawasiliano ili kuboresha utoaji huduma ameitaja namba hiyo maalum kuwa ni 0736 006060 ambayo itatumika kuwasiliana na Baraza kwa jambo lolote.
Aidha, Bi. Mazigo ametanabaisha kuwa, namba hiyo itakuwa ikitumika muda na siku za kazi tu, ambazo ni Jumatatu hadi ijumaa kuanzia saa mbili kamili 02:00 asubuhi hadi 10:30 jioni.
Baraza la Uuguzi na Ukunga ni Mamlaka ya Kisheria inayosimamia wanataaluma na Taaluma za Uuguzi na Ukunga Tanzania, chini ya Sheria ya Mwaka 2010 (The Nursing and Midwifery Act, 2010) ili kuhakikisha huduma zinazotolewa na Wauguzi na Wakunga nchini Tanzania ni za kiwango kinachokubalika na salama kwa jamii.