THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA

TANZANIA NURSING AND MIDWIFERY COUNCIL

Watarajali zaidi ya 700 wamekutana katika Ukumbi wa Chimwaga uliopo Jijini Dodoma kwa lengo la kupata semina elekezi kabla ya kuanza mafunzo kwa vitendo katika maeneo mbalimbali ya kutolea huduma za Afya hapa nchini.

Semina hiyo iliyoandaliwa na Kurugenzi ya Maadili, Usajili na leseni kutoka Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania imelenga kuwajengea uwezo wakutoa huduma kwa kuzingatia kanuni,sheria na miongozo ya taaluma ya Uuguzi na Ukunga hapa nchini.

Akizungumza na watarajali Mkurugenzi wa Huduma za Uuguzi na ukunga hapa Nchini Bi. Ziada Sellah amewakumbusha watarajali hao kuzingatia taratibu za kiuuguzi na Ukunga sambamba na kuwataka kufanya tafiti katika kada hizo.

“Sasa mmeshatoka vyuoni mnakwenda kuhudumia jamii nendeni mkahudumie jamii huku mkufanya tafiti za kutosha katika kada ya Uuguzi na Ukunga hatutegemei ninyi kukaa nyuma nyuma mmeandaliwa, mmeiva sasa nendeni mkafanye kazi”- Bi. Ziada alisema.

Naye Msajili wa Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania Bi. Agnes Mtawa amewasisitiza watarajali hao kuhakikisha wawapo katika maeneo ya kutolea huduma ni vyema kuzingatia miongozo ya sare ili kujitanabaisha baina ya wateja na wanataaluma wengine.

“ Sisi zamani tulipo waona wauguzi na wakunga walituvutia kwa sare zao mpaka tukasema kazi si ndio hii sasa! Maana walivaa mavazi nadhifu na yenye kupendeza nawaombeni mkifika huko mkazingatie sare na hili sio ombi langu ni miongozo ya sare hakikisheni mnazingatia hilo” -Bi. Agnes Mtawa.

Kwa upande wake Mrajisi wa Uuguzi na Ukunga kutoka Zanzibar Bwana Vuai Kombo Haji amewataka watarajali kuhakikisha wanakuwa na matumizi bora ya vifaa vyao vya mawasiliano sambamba na mitandao ya kijamii, huku akiwasisitiza kwenda kujifunza kwa vitendo.

Aidha, Mkurugenzi wa Maadili, usajili na leseni Bi. Jane Mazigo amewataka kuhudhuria siku zote zilizopangwa na Baraza bila ya kukosa ili kuhakikisha wanapata mafunzo mazuri ili kupata weledi wakutosha katika taaluma ya Uuguzi na Ukunga.

Watarajali zaidi ya 700 wanatarajia kuanza mafunzo yao ya vitendo mwanzoni mwa mwezi wa kumi na moja katika vituo 29 hapa nchini ambapo mafunzo hayo yatafanyika kwa jumla ya wiki 52 mfululizo.