Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania (TNMC) limewatunuku wauguzi na wakunga 1222 Leseni na vyeti vya kitaaluma hii leo 13.12.2024 katika Mahafali ya 12 ya kitaaluma yaliyofanyika katika ukumbi wa st.peter’s swaswa uliopo Jijini Dodoma.
Akihutubia katika hafla ya kitaaluma Mgeni rasmi ambaye ni Mkurugenzi wa Huduma za Uuguzi na ukunga nchini na Muuguzi Mkuu wa Serikali Bi.Ziada sellah amewataka wauguzi na wakunga hao kuzingatia maadili ya Uuguzi na Ukunga hapa nchini kwa kufuata miongozo ya kitaaluma.
“sasa leo mmeshatunukiwa vyeti na leseni hatutegemei muuguzi na mkunga kufanya mambo kinyume na miongozo ya kitaaluma mkaihudumie jamii kwa kutoa huduma zenye utu na staha” alisema Bi. Ziada
Katika hatua nyingine Muuguzi Mkuu wa serikali amesisitiza umuhimu wa wataaluma hao kujiendeleza kitaaluma kwani taaluma ya Uuguzi na Ukunga inakuwa kila uchwao.
Naye Msajili wa Baraza la Uuguzi na Ukunga Bi. Agnes Mtawa amesisitiza kwa wauguzi na wakunga kufanya kazi kwa kuzingatia mawanda yao ya kazi, huku akisisitiza kuwa na lugha nzuri wakati wa utoaji huduma za Uuguzi na Ukunga.
“sasa isiwe unafika kwa mgonjwa amelala wewe unamchoma sindano akishituka unamwambia tulia… ulikuwa hujui ni mud awa sindano? Mimi nasema ni vizuri kuwa na lugha nzuri na wateja wetu wakati wa utoaji huduma.” Alisema Bi.Mtawa
Kwa Upande wake Mkurugenzi wa usajili,leseni na Maadili Bi.Jane Mazigo Pamoja na kusisitiza misingi ya maadili kwa wataaluma amewataka wauguzi na wakunga kutumia muda wao mwingi kujifunza ili kuwa wabobezi katika taaluma ya Uuguzi na Ukunga.