THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA

TANZANIA NURSING AND MIDWIFERY COUNCIL


Kwa niaba ya Msajili wa Baraza la Uuguzi na Ukunga, Mkunga Mbobezi na Mratibu wa Mafunzo ya Kujiendeleza Kitaaluma Bi. Mwajuma Mutabazi amekabidhi Cheti cha ithibati ya Moduli sita za mafunzo ya kujiendeleza kitaaluma (CPD) eneo la huduma za dharula kwa wajawazito (Midwifery Emergency Skills Training) kwa Chama cha wakunga Tanzania (TAMA) ambapo amekitaka chama hicho kusimamia misingi ya kitaaluma huku akiahidi kuwa, Ofisi ya msajili ipo wazi muda wote kutoa ushirikiano.

Akipokea cheti hicho rais wa TAMA katika ofisi za chama hicho jijini Dar es salaam, Dkt. Beatrice Mwilike amemshukuru Msajili kwa kuendelea kutoa ushirikiano na kuhakikisha Moduli za mafunzo zinazowasilishwa katika Ofisi yake zinafanyiwa kazi kwa wakati hivyo kurahisisha utekelezwaji wa mafunzo yenye lengo la kuwawezesha wataaluma wa kada ya Ukunga kupata maarifa mapya yatakayowawezesha kuendelea kutoa huduma bora kwa jamii hususani katika eneo la Mama na mtoto.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa TAMA Bwana Nicodem Komba ameshukuru ushirikiano ulipo baina ya chama hicho cha kitaaluma na mamlaka ya usimamizi ambayo ni Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania.

Naye mshauri wa huduma za Ukunga kutoka TAMA Bi. Martha Rimoy pamoja na Katibu Mwenezi wa chama hicho Bi. Agness Nduguru kwa pamoja wameshukuru kupata cheti hicho huku wakiahidi kutoa mafunzo bora ambayo yamethibitishwa na Baraza kwa wakunga wote nchini ambayo licha ya kutoa huduma zenye viwango pia yatawaongezea alama wakati wa uhuishaji wa leseni zao.

Baraza la Uuguzi na Ukunga ni Mamlaka ya Kisheria inayosimamia wanataaluma na Taaluma za Uuguzi na Ukunga Tanzania chini ya Sheria na. 1 ya Mwaka 2010 (The Nursing and Midwifery Act, 2010) na Kanuni zak ili kuhakikisha huduma zinazotolewa na wauguzi na wakunga nchini ni za kiwango kinachokubalika na salama kwa jamii.