THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA

TANZANIA NURSING AND MIDWIFERY COUNCIL

Watarajali zaidi ya 30 wamekutana Jijini Dodoma kwa lengo la kupata semina elekezi kabla ya kuanza mafunzo kwa vitendo katika maeneo mbalimbali ya kutolea huduma za Afya hapa nchini.

Semina hiyo iliyoandaliwa na Kurugenzi ya Maadili, Usajili na leseni kutoka Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania imelenga kuwajengea uwezo wakutoa huduma kwa kuzingatia kanuni, Sheria na miongozo ya taaluma ya Uuguzi na Ukunga hapa nchini.

Akizungumza na watarajali Msajili wa Baraza la Uuguzi na Ukunga hapa Nchini Bi. Agnes Mtawa amewakumbusha watarajali hao kuzingatia taratibu za kiuuguzi na Ukunga sambamba na kuwataka kufanya tafiti katika kada hizo.

“Sasa mmeshatoka vyuoni mnakwenda kuhudumia jamii nendeni mkahudumie jamii huku mkufanya tafiti za kutosha katika kada ya Uuguzi na Ukunga hatutegemei ninyi kukaa nyuma nyuma mmeandaliwa, mmeiva sasa nendeni mkafanye kazi”- Bi. Mtawa.

Bi. Mtawa ameongeza kwa kuwataka watarajali kujitambua katika maeneo yao ya mafunzo huku akiwasisitiza kwenda kujifunza kwa vitendo.

Naye Mkurugenzi wa usajili, Leseni na Maadili TNMC Bi. Jane Mazigo amewasisitiza watarajali hao kuhakikisha wawapo katika maeneo ya kutolea huduma ni vyema kuzingatia miongozo ya sare, kanuni saba za maadili ya taaluma hiyo.

Aidha, Bi. Mazigo amewataka kuhudhuria siku zote zilizopangwa na Baraza bila ya kukosa ili kuhakikisha wanapata mafunzo mazuri ili kupata weledi wakutosha katika taaluma ya Uuguzi na Ukunga.