Maelfu ya wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya Tanzania leo wamejitokeza kwa wingi kushiriki kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Afya Kitaifa 2025, yanayofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete, jijini Dodoma.

Mgeni rasmi katika maadhimisho haya ni Mhe.Waziri wa Afya, Jenista Mhagama , akimuwakilisha Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Tukio hilo kubwa la kitaifa limehudhuriwa na viongozi wa Serikali, wataalamu wa Afya, wadau wa maendeleo, viongozi wa Dini, wanahabari,
wanafunzi wa fani ya Afya, pamoja na wananchi wa kada mbalimbali waliokuwa na kiu ya kujifunza zaidi kuhusu huduma za afya na namna ya kuboresha ustawi wa jamii.
Kaulimbiu ya mwaka huu ni “Tulipotoka, Tulipo, Tunapoelekea; Tunajenga Taifa Imara Lenye Afya”, ikiwa na lengo la kuhimiza jamii kuchukua hatua madhubuti katika kujikinga na magonjwa, kufanya mazoezi, kula lishe bora, na kushiriki kikamilifu kwenye huduma za kinga na tiba.

Maadhimisho haya yameambatana na matukio mbalimbali ya kijamii na kitaalamu yakiwemo midahalo ya kitaaluma, maonesho ya huduma za Afya, uchunguzi wa magonjwa, na matembezi maalum ya kuhamasisha mazoezi ya mwili.
Wiki ya Afya Kitaifaita adhimishwa kila mwaka kama jukwaa la kuhamasisha wananchi kuhusu masuala ya Afya, kuonesha mafanikio ya sekta ya Afya, na kujadili changamoto pamoja na mikakati ya kuimarisha huduma za Afya nchini.