
Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Msajili mapema mwezi juni mwaka huu imewataka wauguzi na wakunga kwa makini na baadhi ya watu wasio na nia njema na taaluma za Uuguzi na Ukunga ambao wanawarubuni wauguzi na wakunga wakiwataka kutoa kiasi cha Fedha ili wawaweze kuwasomewa mafunzo ya kujiendeleza kitaaluma (CPD) jambo ambalo ni kinyume na kifungu cha 27 cha Kanuni ya Mafunzo ya mwaka 2010 pamoja na miongozo ya mafunzo ya taaluma za Uuguzi na Ukunga nchini.
Taarifa hiyo imewataka wauguzi na wakunga nchini, kujiepusha na watu hao na badala yake wajikite kufanya mafunzo katika utaratibu ulioelekezwa kwa kuzingatia vipaumbele vya Taifa pamoja na maeneo yaliyoelekezwa ili kupata alama (CPD Points) kwa mgawanyo uliopo kwenye miongozo ya mafunzo ya kujiendeleza Kitaaluma.
Baraza limetoa ONYO kwa wataaluma na watu wote wenye tabia tajwa hapo juu kuacha mara moja kwani yeyote atakayebainika kufanya hivyo atachukiliwa hatua kali kwa mujibu wa Sheria, taratibu, Kanuni na miongozo ya taaluma ya Uuguzi na Ukunga.
Aidha, Baraza kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) linaendelea kuwafutilia ili kuwabaini wale wote wanaojaribu kuwarubuni na kutapeli Fedha kutoka kwa wauguzi na wakunga kuelekea zoezi la kuhuisha Leseni lenye kundi kubwa la wauguzi na wakunga linalotarajiwa kuanza tarehe 01 Julai 2025.