
Wajumbe wa Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania tarehe 25 Novemba 2025 wamekutana Jijini Dodoma katika ukumbi mdogo wa mikutano wa TANAPA kwa lengo la kufanya Kikao cha robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2025/26.
Kikao kimeongozwa na Mwenyekiti wa Baraza ambaye ni Prof. Lilian Msele huku katibu wake akiwa msajili wa Baraza Bi. Agnes Mtawa.
Pamoja na kujadili ajenda kadhaa, Wajumbe wa Baraza wametoa pongezi kwa sekretarieti ya Baraza kwa usimamizi wa mradi wa ujenzi wa ofisi zinazojengwa Jijini Dodoma eneo la Medeli, Mradi huo unaogharimu kiasi cha Shilingi billioni 1.8 ambapo kwasasa umefikia hatua za mwishoni kukamilika.

Aidha, Wajumbe wa Baraza walitumia wasaha huo kumkaribisha mjumbe mpya ambaye ni Rais wa Chama cha Wauguzi Tanzania (TANNA), Dkt. Ezekiel Mbao, ambapo kwa mujibu wa Sheria ya Uuguzi na Ukunga ya Mwaka 2010 kifungu cha 5.-(1) (e) Sheria imeweka wazi muundo wa wajumbe wa Baraza kuwa, Mwakilishi wa Chama cha Wauguzi Taifa atakuwa ni miongoni mwa wajumbe wa Baraza hili, Dkt. Ezekiel Mbao anachukua nafasi ya kuwa Mjumbe wa Baraza baada ya mtangulizi wake Bw. Alexander Baluhya kumaliza muda wake wa nafasi ya urais ndani ya chama cha wauguzi Tanzania (TANNA).

Ikumbukwe kuwa, kwa mujibu wa Sheria ya Uuguzi na Ukunga ya Mwaka 2010 kifungu cha 5.-(1) (a hadi i) imebainisha muundo wa Baraza kuwa: (a) Mwenyekiti wa Baraza ambae atateuliwa kutoka miongoni mwa wauguzi waandamizi waliosajiliwa; (b) Mkuu wa huduma za Uuguzi na Ukunga nchini; (c) Mwakilishi wa idara ya mafunzo ya Uuguzi kutoka Wizara yenye dhamana na Afya; (d) Mkufunzi muuguzi; (e) Mwakilishi wa Chama cha Wauguzi Taifa; (f) Mwakilishi wa Maafisa Wauguzi wa Mikoa au Wilaya.