Wajumbe wa Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania (TNMC) wakiongozwa na Mwenyekiti wake Prof. Lilian Msele Muuguzi Mbobezi, leo 10 February 2026 wamekutana Jijini Dodoma katika ukumbi mdogo wa mikutano wa Jakaya kwa ajili ya vikao vitavyofanyika kwa siku nne mtawalia maalumu kusikiliza tuhuma mbalimbali zinazowakabili wauguzi na wakunga hapa nchini.
Vikao hivi vinavyoratibiwa na katibu wa Baraza ambaye pia ndiye Msajili wa Baraza Bi. Agnes Mtawa, vinatarajiwa kusikiliza na kufanya maamuzi ya tuhuhuma kumi (10) za kitaaluma zinazowakabili wauguzi na wakunga kutoka mikoa tisa tofauti hapa nchini.

Kwa mujibu wa Sheria ya Uuguzi na Ukunga ya mwaka 2010 kifungu cha 25.-(1) imebainisha makosa ambayo mtaaluma wa uuguzi na ukunga hatakiwi kuyafanya.
Pia, sheria ya Uuguzi na Ukunga 31. -(1) imeweka wazi kuwa mtaaluma ambaye hataridhika na uamuzi wa Baraza anaweza kukata rufaa kwa Waziri wa Afya, ndani ya miezi mitatu toka tarehe ya kupata taarifa ya uamuzi wa Baraza.

Ikumbukwe kuwa, Baraza la Uuguzi na Ukunga ni Mamlaka ya Kisheria inayosimamia wanataaluma na Taaluma za Uuguzi na Ukunga Tanzania, chini ya Sheria ya Uuguzi na Ukunga ya mwaka 2010 iliyorekebishwa mwaka 2023 [The Nursing and Midwifery Act 2010 [CAP 325 R.E 2023] ili kuhakikisha huduma zinazotolewa na Wauguzi na Wakunga nchini Tanzania ni za kiwango kinachokubalika