Author: super-admin

  • NI KOSA KISHERIA KUMTELEKEZA MGONJWA

    NI KOSA KISHERIA KUMTELEKEZA MGONJWA

    “Hakuna mtu anayeweza kuacha kitanda nyumbani aseme mimi nataka nikalale Hospitalini, hivi kweli unaacha kitanda chako cha tano kwa sita, ukalale Hospitali?  Kwa hiyo mara nyingi nasema hii kazi yetu ni ya ubinadamu kwa sababu ni lazima uvae viatu vya mgonjwa na hakuna nayejua yatakayompata dakika mbili kuanzia sasa, unaweza kushitukia na wewe umelazwa na watoa huduma si ni sisi wenyewe, hivi unafikiri tutabadilisha tabia za kutelekeza wagojwa kama tumezoea kutelekeza   tuseme Agness Mtawa, naumwa tumuhudumie vizuri”

    Kauli hiyo imetolewa na Msajili wa Baraza la Uuguzi na Ukunga chini Bi. Agness Mtawa, wakati akiwafundisha Wauguzi na Wakunga wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga Mkoani Pwani, Novemba 13/2023, kuhusu maadili ya taaluma za Uuguzi na Ukunga ikiwa ni muendelezo wa kuwajengea uwezo wataalamu wa sekta hizo mbili.

    Akizungumzia umuhimu wa kuzingatia maadili amewataka wauguzi na wakunga kuzingatia maadili ya taaluma yao, ikiwa ni pamoja na usiri wa taarifa za mgonjwa, kuweka kumbukumbu za wagonjwa, kumshirikisha mgojwa kwa kufafanua aina ya matibabu anayopewa ikiwa ni pamoja na kutomtelekeza mgonjwa.

    Naye Mwanasheria wa Baraza Wakili George Shilla, amewataka Wauguzi na Wakunga Nchini kuhakikisha kila mwanataaluma anakuwa na leseni kabla ya kuanza kutekeleza majukumu ya kitaaluma pamoja na kuwakumbusha Wauguzi na Wakunga waliopo kazini umuhimu wa kuhuisha leseni zao kwa wakati.

    Ikumbukwe kuwa,Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania lilianzishwa mwaka 1953 chini ya sheria ya Wauguzi na Wakunga kwa shabaha ya kusimamia taaluma za Uuguzi na Ukunga ili kuhakikisha jamii inapata huduma iliyosalama huku muuguzi au mkunga anayetoa huduma hapa Nchini lazima awe na leseni ya Baraza, baada ya kuridhika kuwa amefikia viwango vya kitaluuma vinavyokubalika.

  • WAUGUZI NA WAKUNGA NCHINI WATAKIWA KUWA NA LUGHA NZURI KWA WATEJA

    WAUGUZI NA WAKUNGA NCHINI WATAKIWA KUWA NA LUGHA NZURI KWA WATEJA

    Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Maadili,Usajili na Leseni Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania Bi.Jane Mazigo wakati wa mafunzo na sheria ya uuguzi na ukunga yaliyofanyika Halmashauri ya Kibaha katika ofisi za baraza la uuguzi na ukunga mkoani Pwani.

    kwa upande wake Mwanasheria wa baraza la uuguzi na ukunga Tanzania Isaya Nkya wakati wa mafunzo hayo ya sheria na maadili kwa Wauguzi na Wakunga amewataka wauguzi na wakunga wote nchini kuacha tabia ya kumtelekeza mteja kwani kufanya hivyo ni kosa kisheria.

    Ikumbukwe kuwa Wauguzi na wakunga ni sehemu ya kundi kubwa la watoa huduma za Afya, kwa takribani asilimia 60 hadi 80 ambapo wanatakiwa kutoa huduma kwa kuzingatia Maadili, Sheria, kanuni na taratibu ili kuhakikisha jamii inapata huduma bora na Salama.

    Baraza la uuguzi na ukunga Tanzania lipo mkoani pwani kwa siku saba likitajia kuwafikia wauguzi na wakunga wa mkoa huo kwa ajili ya mafunzo ya sheria na maadili kwa wataaluma hao.

  • “ZINGATIENI MAFUNZO KWA VITENDO- BI.MASENGA”

    “ZINGATIENI MAFUNZO KWA VITENDO- BI.MASENGA”

    Wanafunzi wanaosoma taaluma ya Uuguzi na Ukunga katika Vyuo mbalimbali Nchini, wameshauriwa kuzingatia mafunzo kwa vitendo wanapokuwa vyuoni ili kuwa na umahiri unaotakiwa katika taaluma ya Uuguzi na Ukunga pamoja na kufaulu mitihani ya usajili na leseni inayoratibiwa na Baraza.

    Rai hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa mafunzo na maendeleo ya taaluma wa Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania Bi. Happy Masenga, alipozungumza na kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano kwa umma cha Baraza la Uuguzi na Ukunga Jijini Dodoma.

    “Kwa kusema hayo, basi niweze pia kuwashauri wanafumnzi waliopo vyuoni wanaosoma taaluma ya Uuguzi na Ukunga kwamba, wanapokuwa katika mafunzo wazingatie sana kujifunza kwa vitendo katika Hospitali wanazotakiwa kujifunza kwa vitendo, hii inamsaidia sana kuwa na kumbukumbu katika mitihani ya usajili na leseni lakini pia kujenga umahili unaotakiwa”

    Akizungumzia kuhusu vyuo vya uuguzi na Ukunga vilivyosajiliwa kuendesha mafunzo nchini, Mkurugenzi Bi.Masenga, amevitaka Vyuo hivyo kuendesha mafunzo kwa kuzingatia mitaala sanjari na kuwafuatilia wanafunzi wao wanapokuwa katika maeneo ya kujifunza kwa vitendo ili kutoa wauguzi wenye ubora na umahili unaotakiwa.

    Katika hatua nyingine Bi.Masenga, amebainisha awamu tatu za kufanyika kwa mitihani ya leseni kuwa ni Mwezi wa 12, 04, 08 au mwezi wa tisa kwa  kila mwaka wa Fedha wa serikali pia amewataka wahitimu wanaoomba kusajiliwa kufanya mtihani  wa usajili na leseni hususani unaotarajiwa kufanyika mapema mwezi ujao, kuchagua vituo vilivyo karibu na Mikoa wanayoishi na kubainisha vituo saba kuwa ni Pamoja na Taasisi ya Afya na Sayansi Shirikishi Tandabui Mwanza, Chuo Kikuu cha Kampala Dar es Salamu, Chuo cha St. John Dodoma, Chuo cha Stephano Moshi- Kilimanjalo, Chuo cha Afya na Sayansi shiriki – Mbalizi Chuo Kikuu cha Katoliki Iringa (RUCU) Pamoja na  Tabora Polytechnic Mkoani Tabora.

  • WAJUMBE WA BARAZA WAZURU ENEO LA UJENZI WA OFISI ZA TNMC-DODOMA

    WAJUMBE WA BARAZA WAZURU ENEO LA UJENZI WA OFISI ZA TNMC-DODOMA

    Wajumbe wa Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania leo tarehe 03/10/2023 wametembelea eneo la ujenzi wa Ofisi za Baraza.
    Wajumbe hao wakiongozwa na Mwenyekiti wa Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania Profesa Lilian Msele na katibu wa Baraza Bi. Agnes Mtawa, wameonesha kufurahishwa na hatua za awaliza za ujenzi huo.

    Ujenzi huo unatekelezwa na kampuni yenye hadhi ya daraja la kwanza ya Strategic Business Sulution (SBS) ya Jijini Dar es Salaam, ambapo ujenzi huo unaoendelea katika eneo la Medeli-Jijini Dodoma unatarajiwa kukamilika katika kipindi cha miezi kumi (10)

  • TNMC YAENDELEA KUWANOA WAUGUZINA WAKUNGA  NCHINI.

    TNMC YAENDELEA KUWANOA WAUGUZINA WAKUNGA NCHINI.

    Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania limendelea kuwajengea uwezo Wauguzi na Wakunga nchini kwa kuwafundisha jinsi ya kutoa huduma wanaposhiriki zoezi la upasuaji katika chumba cha upasuaji ili kuboresha huduma na mara hii, mafunzo hayo yamefanyika katika Hospitali ya Rufaa ya Ligula Mkoani Mtwara.

     Mafunzo hayo yanayowahusisha Madaktari, Wauguzi na Wakunga pamoja na wahudumu wa Afya wapatao 45 kutoka chumba cha upasuaji, chumba cha wagonjwa wanaohitaji ungalizi karibu, idara ya kusafisha na kutakasa vifaa tiba, sehemu ya huduma za dharura, wodi ya Wazazi sanjari na wodi ya upasuaji.

    Akifafanua juu ya umuhimu wa mafunzo hayo Bi. Salome Kasanga, ambaye ni Muuguzi mtaalamu wa chumba cha upasauaji kutoka Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania amesema, mafunzo hayo yanafanyika chini ya uratibu wa Baraza kwa siku 14 yakiwa na alama 11.4 za mafunzo ya kujiendeleza kazini yakitumia moduli 06 katika usimamizi wa chumba cha upasuaji.

    “Kumekuwa na changamoto ambapo baadhi ya watumishi hawana ujuzi wa kutosha wa kusimamia na kuendesha huduma katika vyumba vya upasuaji hivyo nia ya mafunzo haya ni kuwajengea uwezo ili kuzuia maambukizi kwa wagonjwa wanaofanyiwa upasuaji”

    Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania likiwa ni sehemu ya Taasisi za Wizara ya Afya, lilianzishwa mwaka 1953 ili kusimamia taaluma ya Uuguzi na Ukunga Nchini likiahakikisha kuwa wataalaumu wa kada hizo wanatekeleza majukumu yao kwa kuzingatia weledi na maadili ya taaluma hiyo.