Author: super-admin

  • TNMC: Wauguzi, wakunga zaidi ya 200 wapigwa Msasa Mafunzo ya  Sheria na Maadili Mkoani Morogoro.

    TNMC: Wauguzi, wakunga zaidi ya 200 wapigwa Msasa Mafunzo ya Sheria na Maadili Mkoani Morogoro.

    Timu ya Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania imetoa Mafunzo ya Maadili na Sheria kwa Wauguzi na Wakunga 212 katika Halmashauri ya Mji Ifakara,Kituo cha Afya Kibaoni,Hospitali ya St Fransis,Hospitali ya Kilombero,Wauguzi kutoka Hamashauri Wilaya Mlimba na Chuo cha Uuguzi na Ukunga Edgar Maranta Mkoani Morogoro.

    Ikumbukwe kuwa, Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania ni chombo cha Kisheria kilichoanzishwa chini ya Sheria ya Uuguzi na Ukunga ya 2010, na Kanuni zake kwa ajili ya kutoa, kulinda, kuimarisha, na kuhifadhi Afya ya Jamii, Usalama na Ustawi kupitia usimamizi na Udhibiti wa Shughuli za Mafunzo ya Uuguzi na Ukunga na utoaji wao wa huduma.

    Kwa mujibu wa Sheria hii Baraza lina wajibu wa kuanzisha na kuhakiki viwango vya utendaji, ufanyaji kazi na Maadili yanayotarajiwa kutoka kwa wauguzi na wakunga.

  • TNMC imetangaza Matokeo ya Mtihani wa Usajili na Leseni Uliofanyika Tarehe O7.09.2023.

    TNMC imetangaza Matokeo ya Mtihani wa Usajili na Leseni Uliofanyika Tarehe O7.09.2023.

    Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania (TNMC) linatangaza Matokeo ya Mtihani wa usajili na leseni uliyofanyika tarehe 07.09.2023 Matokeo hayoyanapatikana kwenye akaunti ya kila Mtahiniwa kwenye mfumo wa Baraza (hppts://ww.tnmcis.go.tz).

    Matokeo haya yamechelewa kutangazwa kutokana na baadhi ya watahiniwa kukiuka taratibu za ufanyaji Mitihani ambazo zilizosababisha kufanyika uchunguzi ili kubaini chanzo cha ukiukwaji huo.

    Baraza limekamilisha uchunguzi kwa kushirikiana na vyombo vya usalama na hivyo kufikia maamuzi yafuatayo:-

    1. Kutoa Matokeo ya Mtihani kwa ngazi ya Shahada na Astashahada kwa kuwa hakuna Ushahidi wa ukiukwaji wa taratibu za Mtihani.
    2. Kufuta Mtihani wa ngazi ya Stashahada (Diploma) baada ya kubaini ukiukwaji wa taratibu za Mtihani.
    3. Watahiniwa wote waliofutiwa Mtihani wa ngazi ya Stashahada (Diploma) watarudia Mtihani katika tarehe watakayotangaziwa, hivyo wanashauriwa kufanya maandalizi ya Mtihani huo wa Marudio na hakutokuwa na malipo yoyote kwa Watahiniwa wa Mtihani wa marudio.
    4. Kwa wale wa Shahada na Astashahada ambao hawakufaulu watatakiwa kurudia Mtihani huo kwa utaratibu wa kawaida.
    5. Waliofaulu Mtihani wa Shahada na Astashahada watasajiliwa kwa mujibu wa utaratibu.

    Hata hivyo Msajili wa Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania Bi.Agnes Mtawa amewataka Watahiniwa wote kufuata Taratibu, Kanuni za Mitihani na kuacha njia za mikato ambazo hazina tija na huleta usumbufu usiokuwa wa lazima.

  • Mtihani wa Usajili na Leseni kufanyika Disemba 29,2023

    Mtihani wa Usajili na Leseni kufanyika Disemba 29,2023

    Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania linatarajia kuendesha zoezi la Mtihani mapema siku ya Ijumaa 29/12/2023 kuanzia saa 3:00 asubuhi hadi saa 7:00 mchana, ambapo Jumla ya watahiniwa 4165 wamekidhi vigezo vya kufanya Mtihani huu, wakiwemo waombaji 3917 ambao wanafanya mtihani kwa mara ya kwanza na 248 wanaorudia, kati yao Wanaume ni 1647 na wanawake ni 2518.

    Hayo yamesemwa na Kaimu Msajili Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania Bi. Happy Masenga akizungumza hii leo na vyombo vya habari katika ukumbi wa ofisi za Baraza hilo Jijini Dodoma.

    Aidha, Mtihani huu utafanyika katika vituo vilivyotambuliwa na kukubaliwa na Baraza katika Mikoa ya Mwanza, Dar es Saalam, Dodoma, Kilimanjaro, Mbeya, Iringa na Tabora.

    Lengo la Mtihani huu ni kupima umahiri wa watahiniwa ili kupata wataalamu wa Afya wenye sifa za kusajiliwa na kupewa leseni ya kutoa huduma kama Muuguzi au Mkunga kwa mujibu wa kifungu cha 15 (1) (a-b) cha Sheria ya Uuguzi na Ukunga.

    Mtihani wa usajili na leseni umekuwa ukifanyika tangu kuanzishwa kwa Baraza mwaka 1953 kwa mujibu wa kifungu 6 (a) cha Sheria ambapo hapo awali mtihani huu uliendeshwa kwa ushirikiano kati ya Baraza na Wizara ya Afya.

    Baraza la Uuguzi na Ukunga Nchini lina jumla ya wauguzi na wakunga wenye leseni wapatao 49,994 ambao wanatoa huduma kwenye Hospitali za Rufaa, Mikoa, Wilaya, Vituo vya Afya na Zahanati, idadi hii inajumuisha wauguzi na wakunga walioajiliwa Serikalini pamoja na sekta binafsi kwa ngazi ya Astashahada, Stashahada, Shahada, Uzamili na Uzamivu.

  • Tangazo kwa Watahiniwa wa Mtihani wa Usajili na Leseni Disemba 29.2023

    Tangazo kwa Watahiniwa wa Mtihani wa Usajili na Leseni Disemba 29.2023

    Ofisi ya Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania inawatangazia   watahiniwa wote kufika vituo vya Mtihani wa usajili na leseni siku ya tarehe 28.12.2023 saa mbili asubuhi kwa ajili ya maelekezo.

    Aidha, kadi za indexin vitatolewa siku hiyo kwa ambao hawakuchukua awali, lakini pia namba za Mtihani zitabandikwa kwenye mbao za matangazo zilizopo kituoni hapo na wale ambao hawakukamilisha taratibu za maombi, hawataruhusiwa kuingia kwenye chumba cha Mtihani siku ya Mtihani yaani tarehe 29.12.2023.

    Aidha, watahiniwa wote wanatakiwa kufika kituo cha Mtihani saa moja kamili 01:00 Asubuhi wakiwa wamevaa mavazi nadhifu kwa mujibu wa muongozo wa mavazi kwa watumishi wa umma pia wanatakiwa kuja na vifaa vifuatavyo kwa ajili ya Mtihani; Picha moja (passport size) zenye viwango vilivyoelekezwa, kalamu nyeusi au penseli aina ya HB, ufutio. na kitambulisho kwa watahiniwa wa ngazi ya Shahada na wanaorudia Mtihani. Aidha, kwa watahiniwa wanaofanya kwa mara ya kwanza kwa ngazi ya Stashahada na Astashahada waje na kadi ya Indexin.

  • Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania latoa Msaada wa Kibinadam Hanang

    Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania latoa Msaada wa Kibinadam Hanang

    Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania limepeleka misaada ya kibinadamu katika wilaya ya Hanang palipokumbwa na Maafa ya maporomoko ya tope, Desemba 3 mwaka huu na kusababisha vifo vya watu 89, majeruhi na wengine wakikosa makazi.

    Akikabidhi Misaada hiyo Bw. Augustino Mwita ambaye ni Mkaguzi wa ndani wa Baraza la Uuguzi na Ukunga, amesema watumishi wa Baraza wameguswa na tukio hilo na kuamua kujichanga kutoa faraja kwa waathiriwa kwa kutoa mavazi na vifaa vingine.

    Mkuu wa kitengo cha Huduma za Sheria Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania George Shilla ametoa pole kwa Rais Samia Suluhu Hassan na wana Hanang’ wote kwa janga lililowapata.

    Kwa upande wake, Mkuu wa wilaya ya Hanang’ Janeth Mayanja ameshukuru kwa msaada huo akiwataka wengine waendelee kujitolea haswa vifaa vya ujenzi ili wasio na makazi waweze kujengewa nyumba.

    Hata hivyo serikali na wadau mbalimbali wameendelea kujitokeza na kujitolea misaada mbalimbali ya kibinadamu kwa wahanga hao.

  • TNMC Habari Yazuru Gazeti la Mwananchi.

    TNMC Habari Yazuru Gazeti la Mwananchi.

    Maofisa wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano wa Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania (TNMC) Ndimmyake Mwakapiso na Ezekiel Nyalusi, wameanza ziara ya siku saba ya kuzuru vyombo vya Habari Jijini Dar es Salaam.

    Katika siku ya kwanza leo Disemba 11/2023, kitengo kimefanya ziara katika chumba cha uchakataji wa Habari za Gazeti hilo mashuhuri Nchini.

    Wakiongozwa mwenyeji wao ambaye pia ni Mhariri Mkongwe na mwenye uzeefu wa zaidi ya miaka 20 Rashid Kenjo, Maafisa hao kutoka (TNMC), wamejifunza utendaji kazi wa kilasiku wa chombo hicho na kisha kupitishwa na kupata maelezo ya idara mbalimbali ikiwa ni pamoja na Idara ya habari Mtandao, (Online Media), Kitengo cha Mikakati, Idara ya Magazeti ya Kingereza, Kitengo cha Uhusiano kwa Umma, Idara ya Masoko na mauzo pamoja na kufanya mazungumzo na timu ya Wahariri.

    Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano cha Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania (TNMC) kinafanya ziara hii ya kitaaluma kwenye vyombo vya habari Jijini Dar es Salaamu kwa lengo la kuitangaza Taasisi, kujenga uhusiano na vyombo vya Habari lakini pia kubadilishana uzoefu na umahiri katika suala la kuhabarisha kwa njia ya Mtandao (Online Media)

  • Wataalamu wa Afya watakiwa kuzingatia Mafunzo ya chati Uchungu kupunguza vifo vya Mama na Mtoto

    Wataalamu wa Afya watakiwa kuzingatia Mafunzo ya chati Uchungu kupunguza vifo vya Mama na Mtoto

    Wataalamu wa Afya wametakiwa kutumia taaluma na ueledi walionao kwa kuzingatia mafunzo ya chati uchungu ili kupunguza idadi ya vifo vya Mama na Mtoto ambavyo vimekuwa vikijitokeza.

    Hayo yamesema na Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Daniel Mzee, wakati akizungumza na Madaktari pamoja na Wauguzi Wakunga katika mafunzo ya Chati Uchungu yanayofadhiliwa na USAID kupitia mradi wa Afya Yangu yanayoendelea Mkoani Shinyanga.

    Dkt. Mzee amewaeleza wataalamu hao kuwa mafunzo hayo yana umuhimu mkubwa katika kuboresha Afya ya Mama na Mtoto, hivyo na ili kufanyika vizuri hawana budi kuyazingatia kwa kuyafanyia kazi kwa makini.

    “Tusikilize vizuri mafunzo na tuzingatie miongozo kwa lengo la kupunguza vifo vya mama na mtoto. Bado kasi haijawa ya kuridhisha, lakini hapa tulipofikia ni pazuri hivyo tuendelee kupambana, Nina uhakika mtakapoenda kwenye maeneo yenu ya kazi mtatumia mafunzo haya kuwafundisha na wenzenu ili mboreshe huduma nzuri hususani katika kuokoa maisha ya mama na mtoto”, amesema Dkt. Mzee.

    Kwa upande wake Mkunga Mbobezi kutoka Idara ya Huduma za Uuguzi na Ukunga Wizara ya Afya, Aziza Machanje, amesema Serikali imeelekeza kutolewa kwa mafunzo ya Chati Uchungu ambayo imeboreshwa zaidi kuzidi kukabiliana na changamoto zitokanazo na uzazi hasa kwa mama na mtoto.

    “Chati Uchungu ni chati inayotumia kuangalia maendeleo ya mama mjamzito wakati wa kujifungua ili kujua maendeleo ya mama na mtoto tumboni, Tumeona umuhimu mkubwa wa kuwa nayo moja ili itumike nchini kote, na ndiyo maana Wizara imeamua kuandaa haya mafunzo kwa wataalamu wetu wa Afya”, amesema Machanje.

    Credit: WAF

  • Ummy aagiza Daktari na Muuguzi kuchukuliwa hatua

    Ummy aagiza Daktari na Muuguzi kuchukuliwa hatua

    Waziri wa Afya Ummy Mwalimu ametaka Mabaraza ya Madaktari na Wauguzi kuwachukulia hatua Mganga na Muuguzi waliosababisha kifo cha mjamzito Mariam Zahoro kilichotokea Kituo cha Afya Kabuku, Wilaya ya Handeni mkoani Tanga.

    Mwalimu amesema Mariam hakufariki kwa ajili ya kukosa kiasi cha shilingi 150,000, bali ni kwa ajili ya uzembe wa baadhi ya wahudumu wa Afya kwa kushindwa kuwajibika kutokana na hali aliyokuwa nayo mgonjwa.

    Ameyasema hayo Novemba 27, 2023 baada ya kupokea taarifa ya Tume iliyoundwa kuchunguza jambo hilo lililotokea Novemba 11, mwaka huu, kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Kituo cha Afya Kabuku, ambapo Tume imebaini wahudumu wawili ndiyo wenye makosa.

    “Tunataka Mabaraza ya Madaktari na Wauguzi wachukue hatua kwa Daktari na Muuguzi walioshindwa kuwajibika,kosa la daktari ni kushindwa kufika kwa wakati tayari ameelezwa hali ya mjamzito ni mbaya,hata alipofika, alishindwa kuchukua hatua ya kumpeleka Hospitali ya Wilaya ya Handeni, Mkata baada ya kumkosa Muuguzi wa dawa za usingizi ili mgonjwa afanyiwe upasuaji lazima apewe dawa za usingizi,”ameeleza Mwalimu na kuongeza kuwa

    “Kosa la Muuguzi ni kumueleza mgonjwa anatakiwa alipe 150,000 wakati huo sio utaratibu, kwani alitakiwa atoe huduma bila kudai fedha hizo hivyo nitangaze mjamzito hakupoteza maisha kwa ajili ya kukosa sh.150,000, bali ni kwa ajili ya uzembe wa baadhi ya wahudumu wa Afya,”.

    Mwalimu amesema Sera ya Afya ya mwaka 2007 inamtaka mjamzito kupata huduma bila malipo, hivyo amepinga makubaliano yaliyofikiwa kwenye kata kati ya wahudumu wa Afya na watendaji akiwemo Diwani wa eneo hilo kupitisha kuwa mjamzito atatoa sh. 150,000 kwa ajili ya upasuaji.

    Amesema anataka Mabaraza hayo yatoe maamuzi ndani ya wiki mbili, huku akiwaahidi wananchi hao kuwa wahudumu hao wawili hawatarudi Kabuku na kutaka hatua kali zichukuliwe dhidi yao iwe onyo kwa wengine.

    Hata hivyo Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amekiri baadhi ya majengo kwenye kituo hicho yamechoka, na atatafuta fedha kujenga mengine.

    Credit:Gazeti la Majira

  • TNMC YAWAPIGA MSASA WAUGUZI,WAKUNGA NAMNA YA KUSHIRIKI UTOAJIHUDUMA KATIKA CHUMBA CHA UPASUAJI – NDANDA.

    TNMC YAWAPIGA MSASA WAUGUZI,WAKUNGA NAMNA YA KUSHIRIKI UTOAJIHUDUMA KATIKA CHUMBA CHA UPASUAJI – NDANDA.

    Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania limeendesha Mafunzo ya namna ya kushiriki utoaji huduma katika chumba cha upasuaji kwa Wauguzi na Wakunga katika Hospitali ya St. Benedict iliyopo Ndanda – Halmashauri ya Masasi,Mkoani Mtwara ambapo washiriki walikuwa ni Wauguzi na Wakunga, wataalamu wa dawa za usingizi na ganzi pamoja na Madaktari wa upasuaji. 

    Akitoa mafunzo hayo Afisa Muuguzi Mbobezi Kitengo Cha Upasuaji Bi. Salome Kassanga amewataka watumishi yale waliyoyapata kutoka katika mafunzo hayo ili kuhakikisha jamii inapata huduma iliyo bora na salama.

    Kwa upande wake Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo Dr. Isaiah Michael Sienz amesema mafunzo hayo yamesaidia kuboresha mazingira ya vyumba vya upasuaji na kuwaongezea ujuzi watumishi hao ambapo hapo awali hawakuwa na ujuzi huo kutokana na kutosoma namna ya kutoa huduma ya aina hiyo, baada ya mafunzo kusitishwa hapa nchini.

    Pamoja na mafunzo hayo Dr.Sienz amemshukuru Msajili wa Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania Bi.Agnes Mtawa kwa jitihada za utoaji wa mafunzo ya aina hiyo kwa watumishi waliopo kazini huku akiiomba serikali irudishe mafunzo hayo ili kuboresha utoaji wa huduma ya aina hiyo kwa wateja mbalimbali.

    Mafunzo hayo yaliyohudhuriwa na wauguzi na wakunga zaidi ya 40 pamoja na wauguzi watarajali yanatarajiwa kuwa chachu ya utoaji wa huduma bora Mkoani Mtwara.

  • MSAJILI WA BARAZA LA UUGUZI NA UKUNGA TANZANIA ATUA MAFIA

    MSAJILI WA BARAZA LA UUGUZI NA UKUNGA TANZANIA ATUA MAFIA

    MAFIA- Timu ya Maofisa wa Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania wakiongozwa na Msajili wa Baraza Bi. Agnes Mtawa, mapema leo wamezuru Ofisi ya Mkuu wa Wilaya wa kisiwa cha Mafia kwa lengo la kujitambulisha kabla ya kuanza zoezi la utoaji Elimu ya Sheria na Maadili kwa wauguzi na wakunga wa Wilaya ya Mafia iliyopo Mkoani Pwani.

    Ikumbukwe kuwa Maofisa wa Baraza hilo wapo mkoani Pwani kwa ziara ya siku nane katika Halmashauri zote za Mkoa huo.