Author: super-admin

  • TAARIFA YA MATOKEO YA MTIHANI WA USAJILI NA LESENI ULIOFANYIKA TAREHE 23.08.2024

    TAARIFA YA MATOKEO YA MTIHANI WA USAJILI NA LESENI ULIOFANYIKA TAREHE 23.08.2024

    Msajili wa Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania Bi.Agnes Mtawa anawajulisha kuwa matokeo ya Mtihani wa usajili na leseni uliofanyika tarehe 23 Agosti, 2024 yametolewa tarehe 07 Novemba, 2024 baada ya kukamilisha mchakato wa taratibu za kisheria kwa mujibu wa Sheria ya Uuguzi na Ukunga Tanzania ya mwaka 2010 (The Nursing and Midwifery Act.2010).


    Taarifa iliyotolewa na Msajili imeeleza kuwa, Matokeo hayo yametolewa kupitia akaunti ya mtahiniwa iliyopo kwenye mfumo wa kumbukumbu wa Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania (TNMCIS). Hivyo, kila mtahiniwa atembelee akaunti yake katika mfumo wa Baraza https://tnmcis.tnmc.go.tz. na kuweza kuona matokeo yake.
    Kwa ambao wameshindwa Mitihani huu, wanajulishwa kuwa tarehe ya kurudia mtihani kwa kipindi kingine itakuwa tarehe 20 Desemba, 2024.


    Taratibu za maombi zimeelekezwa katika tovuti ya Baraza.
    Aidha, Baraza linaomba radhi kwa kuchelewa kutoa matokeo haya na kwa usumbufu uliojitokeza kwa kipindi hiki cha kusubiria matokeo, Taarifa ya msajili imeeleza

  • WATARAJALI WAPATA SEMINA ELEKEZI KABLA YA KUANZA MAFUNZO KWA VITENDO.

    WATARAJALI WAPATA SEMINA ELEKEZI KABLA YA KUANZA MAFUNZO KWA VITENDO.

    Watarajali zaidi ya 700 wamekutana katika Ukumbi wa Chimwaga uliopo Jijini Dodoma kwa lengo la kupata semina elekezi kabla ya kuanza mafunzo kwa vitendo katika maeneo mbalimbali ya kutolea huduma za Afya hapa nchini.

    Semina hiyo iliyoandaliwa na Kurugenzi ya Maadili, Usajili na leseni kutoka Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania imelenga kuwajengea uwezo wakutoa huduma kwa kuzingatia kanuni,sheria na miongozo ya taaluma ya Uuguzi na Ukunga hapa nchini.

    Akizungumza na watarajali Mkurugenzi wa Huduma za Uuguzi na ukunga hapa Nchini Bi. Ziada Sellah amewakumbusha watarajali hao kuzingatia taratibu za kiuuguzi na Ukunga sambamba na kuwataka kufanya tafiti katika kada hizo.

    “Sasa mmeshatoka vyuoni mnakwenda kuhudumia jamii nendeni mkahudumie jamii huku mkufanya tafiti za kutosha katika kada ya Uuguzi na Ukunga hatutegemei ninyi kukaa nyuma nyuma mmeandaliwa, mmeiva sasa nendeni mkafanye kazi”- Bi. Ziada alisema.

    Naye Msajili wa Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania Bi. Agnes Mtawa amewasisitiza watarajali hao kuhakikisha wawapo katika maeneo ya kutolea huduma ni vyema kuzingatia miongozo ya sare ili kujitanabaisha baina ya wateja na wanataaluma wengine.

    “ Sisi zamani tulipo waona wauguzi na wakunga walituvutia kwa sare zao mpaka tukasema kazi si ndio hii sasa! Maana walivaa mavazi nadhifu na yenye kupendeza nawaombeni mkifika huko mkazingatie sare na hili sio ombi langu ni miongozo ya sare hakikisheni mnazingatia hilo” -Bi. Agnes Mtawa.

    Kwa upande wake Mrajisi wa Uuguzi na Ukunga kutoka Zanzibar Bwana Vuai Kombo Haji amewataka watarajali kuhakikisha wanakuwa na matumizi bora ya vifaa vyao vya mawasiliano sambamba na mitandao ya kijamii, huku akiwasisitiza kwenda kujifunza kwa vitendo.

    Aidha, Mkurugenzi wa Maadili, usajili na leseni Bi. Jane Mazigo amewataka kuhudhuria siku zote zilizopangwa na Baraza bila ya kukosa ili kuhakikisha wanapata mafunzo mazuri ili kupata weledi wakutosha katika taaluma ya Uuguzi na Ukunga.

    Watarajali zaidi ya 700 wanatarajia kuanza mafunzo yao ya vitendo mwanzoni mwa mwezi wa kumi na moja katika vituo 29 hapa nchini ambapo mafunzo hayo yatafanyika kwa jumla ya wiki 52 mfululizo.

  • TNMC YAZINDUA MFUMO WA MAWASILIANO KWA WATEJA

    TNMC YAZINDUA MFUMO WA MAWASILIANO KWA WATEJA

    Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania (TNMC) leo 11.10.2024 limezindua mfumo wa mawasiliano ya huduma kwa wateja utakao tumika kuwasiliana na umma hususani wadau wake wakuu ambao ni wauguzi na wakunga ndani na nje ya nchi ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha kilele cha wiki ya huduma kwa wateja.

    Wiki ya huduma kwa wateja ilianza tarehe 07 Oktoba 2024 na kumalizika leo Oktoba 11, 2024 ikiwa imebeba kauli mbiu inayosema “Huduma zenye ubora na za kiwango cha juu zaidi”.
    Akizindua mfumo huo wa mawasiliano katika ofisi za Baraza Jijini Dodoma kaimu Msajili Bi. Jane Mazigo, amesema kwa sasa Baraza litakuwa linatumia namba moja tu ya mawasiliano ili kuboresha utoaji huduma ameitaja namba hiyo maalum kuwa ni 0736 006060 ambayo itatumika kuwasiliana na Baraza kwa jambo lolote.

    Aidha, Bi. Mazigo ametanabaisha kuwa, namba hiyo itakuwa ikitumika muda na siku za kazi tu, ambazo ni Jumatatu hadi ijumaa kuanzia saa mbili kamili 02:00 asubuhi hadi 10:30 jioni.

    Baraza la Uuguzi na Ukunga ni Mamlaka ya Kisheria inayosimamia wanataaluma na Taaluma za Uuguzi na Ukunga Tanzania, chini ya Sheria ya Mwaka 2010 (The Nursing and Midwifery Act, 2010) ili kuhakikisha huduma zinazotolewa na Wauguzi na Wakunga nchini Tanzania ni za kiwango kinachokubalika na salama kwa jamii.

  • CHAMA CHA “WANAFIZIOTHERAPI” CHA ITEMBELEA OFISI YA  MSAJILI TNMC.

    CHAMA CHA “WANAFIZIOTHERAPI” CHA ITEMBELEA OFISI YA MSAJILI TNMC.

    Viongozi wa Chama cha “wanafiziotherapi” Tanzania (Association of Physiotherapists in Tanzania) leo oktoba 10,2024 wameitembelea ofisi ya Msajili wa Baraza la Uuguzi na Uunga Tanzania kwa lengo la kujifunza mambo mbalimbali ya utendaji kazi wa TNMC.

    Pamoja na mambo mengine mengi Viongozi hao ndg. Jerusalem Makotore(kulia) ambaye ni Mhazini na Dietrich Chussi(kushoto) ambaye ni katibu wameonesha kufurahia mapokezi hayo waliyoyapata kutoka ofisi ya Msajili.

    Kaimu Msajili Bi. Jane Mazigo amewapongeza wataalam hao kwa kutembelea Ofisi ya Msajili na kuwaeleza namna Baraza linavyosimamia taaluma na kuhakikisha jamii inapata huduma bora aidha, amewakaribisha kwa wakati mwingine watakapohitaji kujifunza zaidi.

    Ikumbukwe kuwa, Baraza la Uuguzi na Ukunga ni Mamlaka ya Kisheria inayosimamia wanataaluma na Taaluma za Uuguzi na Ukunga Tanzania, chini ya Sheria ya Mwaka 2010 (The Nursing and Midwifery Act, 2010) ili kuhakikisha huduma zinazotolewa na Wauguzi na Wakunga nchini Tanzania ni za kiwango kinachokubalika na salama kwa jamii.

  • ‘Leseni Kwa Muuguzi, Mkunga ni Kibali Cha Utoaji Huduma- Bi.Jane Mazigo.

    ‘Leseni Kwa Muuguzi, Mkunga ni Kibali Cha Utoaji Huduma- Bi.Jane Mazigo.

    “Leseni ni utambulisho kwa muuguzi na mkunga kutoa huduma kwa jamii na ipo kwa mjibu wa Sheria ya Uuguzi na Ukunga ya mwaka 2010 hivyo, ni vyema kwa Muuguzi na Mkunga kuwa na leseni iliyo hai muda wote wa kutoa huduma”.

    Hayo ameyasema Bi.Jane Mazigo,  Mkurugenzi wa Maadili, Usajilina Leseni akizungumza na TNMC Habari mapema tarehe 19 septemba 2024.

    Bi. Mazigo, ameongeza kuwa kwa mujibu wa Sheria ya Uuguzi na Ukunga kifungu cha 21 (A) na (B) Sheria inafafanua majukumu ya msajili wa TNMC kuwa ni kumsajili Muuguzi na Mkunga na kumpa leseni pamoja na kuhuisha leseni hiyo mara inapokwisha muda wake kwa mujimu wa miongo ya Baraza.

    “pia kwa mujibu wa Sheria ya Uuguzi na Ukunga kifungu cha 38 inaeleza adhabu ambazo muuguzi na mkunga atakumbana nazo pindi atakapobainika akitoa huduma pasipo kuwa na leseni hai” alisema Bi.Mazigo

    Katika hatua nyingine Bi.Mazigo, amewakumbusha waajiri wa wauguzi na wakunga kote nchini, kuhakikisha wanazingatia leseni kwa wataaluma hao kabla ya kuwaajiri kwani ni kosa kisheria kwa mwajiri kumwajiri mtoa huduma za Uuguzi na Ukunga pipokuwa na leseni na utaratibu huu ni wa kimataifa na unalengo la kulinda Afya ya Jamii zinazopokea huduma duniani kote.

    Zaidi ya wauguzi 6,000 wanatakiwa kuhuisha leseni zao katika kipindi cha kuanzia tarehe 01 Julai mpaka 30 Disemba 2024 kwa gharama za kawaida na baada ya muda huo kupita mfumo utaanza kutoza pamoja na penati, hivyo wauguzi wote mnaofahamu kuwa mnatakiwa kuhuisha leseni ni vema mkatumia muda ulibainishwa kuhuisha leseni zenu pasipo kusahau kuwa na alama muhimu za kujiendeleza kitaaluma yaani CPD Point.

  • TNMC Kuanzisha Kituo Cha Mawasiliano , Kuboresha Utoaji Huduma Kwa Mteja.

    TNMC Kuanzisha Kituo Cha Mawasiliano , Kuboresha Utoaji Huduma Kwa Mteja.

    SASA KUTUMIA NAMBA MOJA YA MAWASILIANO.

    Katika kuboresha huduma kwa mteja, Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania TNMC linaendelea na mchakato wa kunzisha kituo cha mawasiliano na wadau wake hususani wauguzi na wakunga nchini na duniani kwa ujmla, machakato ambao unatarajiwa kukamilika na kuanza kutumika mapema mwezi huu Oktoba 2024.

    TNMC Inajenga mfumo huu wa mawasiliano baada ya kuwepo kwa changamoto kadhaa kwa mfumo wa sasa ambao mtu anayewasiliana na Baraza analazimika kutumia namba binafsi za Maafisa waliopo kwenye kurugenzi na vitengo kushugulikia masuala mbalimbali kama vile usajili na leseni, Mitihani, Indexsing na majukumu ya Baraza kwa ujumla.

    Mapema Septemba 19.2024 mtaalamu kutoka kampuni ya simu ya TTCL alitoa mafuzo kwa maafisa wa TNMC yaliyolenga kuwajengea uwezo wa namna ya kuutumia wakati wa kuwasiliana na miongoni mwa mambo mazuri na ya msingi yaliyofundishwa ni pamoja na Mawasiliano hayo sasa yatatumia kompyuta mpakato badala ya simu, wateja zaidi ya watano wanaweza kupiga simu kwa kutumia namba moja maalum itakayoteuliwa ambapo, mteja anaweza kuipiga kupitia mtandao wowote.

    Mfumo pia utakuwa na uwezo wa kumuelekeza mpigaji Ofisi sahihi ya kushughulikia huduma anayohitaji, mfumo utakuwa na uwezo wa kurekodi mazungumzo ya Mteja na Mtoa huduma kwa ajili ya rejea, lakini pia mfumo huu wa mawasiliano utakuwa na uwezo wa kumwelekeza mtoa huduma jinsi ya kutatua changamoto nazokutananazo. Mf. Namna ya kutengeneza neno la siri (Password) kwa waliosahau pasipo kuongea na mtoa huduma.

    TNMC kupitia mkataba wake wa huduma kwa mteja, mara zote imedhamilia kutoa huduma bora kwa umma hususani wauguzi na wakunga wanapofika ofisini au kwa njia ya mawasiliano kwa shabaha ya kudumisha uhusiano chanya jambo ambalo litachangia jamii ipate huduma bora na salama.

  • TNMC Yashiriki Mkutano wa ECSACON Lesotho

    TNMC Yashiriki Mkutano wa ECSACON Lesotho

    TNMC ikiwakilishwa na Msajili Bi. Agnes Mtawa, pamoja na maafisa waandamizi  ambao ni Salome Kassanga na Irene Chilewa, imeshiriki Mkutano wa kimataifa wa kisayansi unaoratibiwa na jumuiya ya ECSACON  nchini Lesotho  kuanzia tarehe 11 hadi 13 Septemba 2024 kwa lengo la kubadilishana  elimu, uzoefu na kuboresha utoaji huduma katika sekta ya Afya kwa nchi wanachama.

    Mkutano huo unaotoa fursa kwa washiriki kujifunza, kufahamiana na kubadilishana uzoefu katika utoaji wa huduma za Afya, uelimishaji wa Uuguzi, Wadhibiti, Serikali na vyama vya kitaaluma , huandaliwa kila baada ya miaka miwili  katika nchi mabalimbali wanachama ambapo Tanzania ni miongoni mwa nchi hizo.

    Jumla ya nchi 16 wanachama zinazounda jumuia ya ECSACON ni pamoja na Tanzania, Botswana, Kenya, Lesotho, Malawi, Mauritius, Msumbiji, Namibia, Rwanda, Seychelles, Afrika Kusini, Sudan Kusini, Swaziland, Uganda, Zambia na Zimbabwe.

    ECSACON ilianzishwa mwaka wa 1990 kama chombo cha utekelezaji cha iliyokuwa Sekretarieti ya Jumuiya ya Madola ya Afrika Mashariki, Kati na Kusini (CRHCS-ECSA) katika eneo la Uuguzi na Ukunga chenye makao yake makuu Jijini Arusha nchini Tanzania, ambayo sasa inajulikana kama Jumuiya ya Afya ya ECSA (ECSA HC) ikiwa na majimbo 14 ya kikanda. Pia, ni mojawapo kati ya vyuo vitano vya ECSA-HC ambavyo ni COSECSA ,CANECSA, COPECSA na ECSACOG.

  • Msajili TNMC akiwasilisha taarifa ya utendaji kazi wa TNMC mbele ya kamati ya Bunge.

    Msajili TNMC akiwasilisha taarifa ya utendaji kazi wa TNMC mbele ya kamati ya Bunge.

    Msajili wa Baraza la Uuguzi na Ukunga nchi Tanzania Bi. Agnes Mtawa akiwa na menejimenti yake, tarehe 06 Agosti 2024 aliwasilisha taarifa ya utendaji kazi wa Baraza mbele ya kamati ya Bunge inayosimamia sekta ya Afya na UKIMWI kupitia kikao kilichofanyika katika ukumbi mdogo wa Bunge Bungeni Jijini Dodoma.

    Kamati hiyo ambayo iliongozwa na Mwenyekiti wake Mhe. Elibariki Kingu (MB) kwa ujumla wamefurahishwa na wasilisho la Msajili na kubainisha kuwa wasilisho hilo limesababisha wabunge wa kamati hiyo kulifahamu vema Baraza pamoja na mipango yake.

    Kwa kweli tuwapongeze sana Baraza kwa utendaji mzuri wa kazi na pia nikupongeze sana Dada Agnes, kwa kweli unaonesha jinsi gani unaijua taasisi unayoiongoza, CMO huyu ni hazina ya Wizara ya Afya endeleeni kumtumia kwa mambo mengi” Alisema Mwenyekiti wa kamati hiyo Mhe. Elibariki Kingu.

    Aidha, baada ya wasilisho hilo wabunge ambao ni wajumbe wa kamati hiyo, waliuliza maswali mbalimbali yenye nia ya kulielewa Baraza na majukumu yake, mipango yake na maendeleo yaliyofikiwa tangu kuanzishwa kwake mwaka 1953, maswali yote yalijibiwa vema na Msajili na hata Mwenyekiti wa kamati kumpongeza kwa umahiri wa kufafanua.

  • “ONGEZENI KASI YA UTOAJI WA HUDUMA ZA UUGUZI NA UKUNGA”-Waziri Mhagama.

    “ONGEZENI KASI YA UTOAJI WA HUDUMA ZA UUGUZI NA UKUNGA”-Waziri Mhagama.

    Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama ameitaka Idara ya Uuguzi na Ukunga kuongeza kasi ya utoaji wa huduma za uuguzi na ukunga pamoja na kufuatilia ubora wa kazi hizo ili mwananchi apate huduma iliyobora.

    Waziri Mhagama amesema hayo Septemba 5, 2024 wakati wa kikao na Idara ya Uuguzi na Ukunga kwa ajili ya kujitambulisha na kujadili utendaji kazi wa Idara hiyo katika Wizara ya Afya.

    “Hakuna jambo ambalo linakera unapokutana na muunguzi au mkunga anaeshindwa kutekeleza wajibu wake kwa jambo la msingi la kutetea uhai wa mgonjwa pindi anapoitaji huduma yake.”Amesema Waziri Mhagama

    Aidha Waziri Mhagama amesema mtumishi hatakiwi kuwa na presha, anatakiwa apewe haki zake zote za msingi ili mtumishi huyo azingatie wajibu wake wa kumhudumia mgonjwa na kuokoa maisha yake.

    Awali Wakati akitoa taarifa ya Idara ya Uuguzi na Ukunga akimwakilisha Mkurugenzi wa idara hiyo bwana Saturini Manangwa amesema idara hiyo imefanikiwa Kuimarisha ubora wa huduma za akina mama kabla, wakati na baada ya kujifungua kwa kuanzisha huduma mwambata kwenye vyumba vya kujifungulia ambapo hadi sasa jumla ya vituo 41 vimeanzisha utoaji wa huduma hiyo

    Bwana Manangwa amesema, miongoni mwa majukumu ya idara hiyo ni pamoja na kuimarisha ubora wa huduma za Uuguzi na Ukunga katika ngazi zote za vituo vya kutolea huduma vya umma na binafsi, Kutoa ushauri wa kimkakati kwa Serikali kuhusu huduma za Uuguzi na Ukunga katika mfumo wa sekta ya afya.

    “Majukumu yetu mengine ni kuhamasisha matumizi ya tafiti na kuwa na huduma linganifu pamoja na Kuimarisha ushirikiano na wadau wote ngazi ya Taifa, Kanda na Kimataifa, kusimamia mafunzo mahala pa kazi kwenye huduma za Uuguzi na Ukunga.” Amesema Bw. Manangwa

    Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama ameambatana na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Afya Ndg. Ismail Rumatila ambapo ameendelea kukutana na Idara mbalimbali za Wizara ya Afya kwa lengo la kutambua majukumu ya Idara pamoja na kujadili namna ya utendaji kazi wa Idara hizo.

  • Dkt. Ndugulile Rasmi ni Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika.

    Dkt. Ndugulile Rasmi ni Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika.

    Dkt. Faustine  Ndugulile amechaguliwa Agosti 27, 2024 na wajumbe wa Kikao cha 74 cha WHO kanda ya Afrika kushika nafasi hiyo kuanzia Agosti 27, 2024 aliyepokea kijiti kutoka kwa Dkt. Matshidiso Moeti wa Bostwana ikiwa ni kwa mara ya Kwanza Tanzania inachukua nafasi hiyo.

    Dkt. Ndugulile ambaye ni Mbunge wa Kigamboni (CCM), Katika kinyang’anyiro hicho amewashinda wagombea wengine walikuwa ni pamoja na Dk Boureima Hama Sambo (Niger) Dkt. N’da Konan Michel Yao (Cote d’Ivoire) Dkt. Ibrahima Soc’e Fall (Senegal) na Dkt. Richard Mihigo (Rwanda).

    Dkt. Ndugulile amepata ushindi huo baada ya nchi 19 kuipigia kura Tanzania katika mzunguko wa kwanza, 12 wakiipigia Senegal, saba (Niger) na nchi saba zikiipigia Rwanda.

    Matokeo hayo yametolewa Agosti 27, 2024 katika Mkutano wa Afya wa 74 wa Shirika la Afya Duniani (WHO) uliofanyika  Brazzaville, nchini Congo.

    Mzunguko wa pili wa kuondoa mgombea mmoja, mgombea kutoka Niger alipigiwa kura 22 za kuondolewa, Rwanda kura 20 na Absteein alipigiwa kura tatu.
    Katika matokeo ya jumla ya mzunguko wa pili Dk Ndugulile alipata kura 25, Senegal 14 na Niger kura sita.
    Dk Ndugulile ambaye ni mwanateknolojia, mtunga sera, mwanasiasa na mwakilishi wa wananchi, aliwakilisha nchi baada ya kuteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuwania kinyang’anyiro hicho.
    Kura hizo zimepigwa na Mawaziri wa Afya kutoka Kanda ya Afrika walioanza mkutano huo baada ya kufunguliwa na Rais wa Congo, Denis Sassou Ng’uesso.

    Mkurugenzi mpya wa Shirika la Afya Duniani Kanda ya Afrika (WHO – AFRO) Dkt. Ndugulile amewashukuru wadau wa Afya nchini waliomsaidia katika kampeni ya kuwania nafasi hiyo kwa njia ya mtandao.

    Dkt. Ndugulile ameahidi utumishi uliotukuka kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kuendelea kuboresha Sekta ya Afya huku akitaja maeneo yenye changamoto Afrika kama ongezeko la vifo vitokanavyo na magonjwa yasiyokua ya kuambukiza, ukosefu wa chanjo na vifo vya akina mama na watoto ikiwa ni kipaumbele chake katika kuhakikisha utatuzi wake unafanyika ipasavyo.

    Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama pamoja na kumpongeza Dkt. Ndugulille kwa ushindi huo, Mhe. Mhagama, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuridhia na kupitisha Jina la Dkt. Faustine Ndugulile kuipeperusha vyema Bendera ya Tanzania katika uchaguzi huo pamoja na juhudi alizozifanya katika kufanikisha ushindi huo.